Tuesday, August 19, 2014

AGANO JIPYA JUU YA ADUI ZETU-Mch.Lugano Mwakisole


MCHUNGAJI LUGANO MWAKISOLE

AGANO JIPYA JUU YA  ADUI ZETU.
(Math.5:43-47)

Leo ninapenda tushirikishane mtazamo wa agano jipya juu ya adui zetu.
Mtazamo wa agano la kale na agano jipya ni tofauti.Agano la kale(torati)kwa sehemu linasema  jino kwa jino au linaruhusu kulipa baya kwa baya lakini ni tofauti na agano jipya linaagiza kuwatendea mema adui zetu.Si kwamba biblia inapingana,kila watu walipewa maagizo na namna ya kuishi kwa wakati wake.sisi tupo kipindi cha agano jipya na maagizo ya Yesu aliyoyatoa ni tofauti na ya kale.

Maagizo tuliyopewa ni magumu zaidi na hii inatokana na pia tuna uwezo mkubwa wa kushinda sababu tuna neema zaidi kutokana na ukombozi wa Yesu pia tuna Roho Mtakatifu aliyemwagwa kwa wote tofauti na zamani ilikuwa kwa watu maalumu.Daudi aliweza kusamehe na kumpenda adui yake sababu alikuwa na Roho mtakatifu lakini ilikuwa ngumu kwa wafuasi wake kuelewa sababu walihishi kwa sheria na kufuata maongozi ya Daudi lakini wenyewe hawakujazwa Roho.Tofauti na sasa kila mtu amejaa Roho hivyo anawezeshwa kushinda vikwazo na kusamehe pia kuwapenda adui kutokana na nguvu ya Roho mtakatifu iliyo ndani yetu.(waefeso 3;20)Si vema katika vipengele vigumu kukwepa maagizo ya agano jipya na kukimbilia la kale ili kujifariji.Wengi wetu wanalipa kisasi na kujitetea kupitia maandiko na wengine wanalaani na kutoa maneno ya laana pengine hata madhabahuni na kutafuta maandiko ya kuwafariji.Biblia yapasa kuielewa kwa upana na kujifunza kwa umakini,si kila andiko utalitumia kwa wakati huu.mengine yaweza kusomwa kama historia au unabii uliopita,mengine ni ya sasa na yanahitaji kutekelezwa na mengine ni unabii ujao yapasa uyajue lakini usitumie kwa sasa kama utekelezaji utasababisha ajali katika uliwengu wa roho.Lakini yote tumewekewa ili tujifunze na tukiyaelewa yatatufaa.

Mtazamo wa sasa juu ya adui zetu ni;
(a)kupenda adui zetu(mathayo 5;44)
Upendo wetu tunarithishwa na Yesu.aliwapenda adui hata siku moja mbaya wake amebeba panga ili amkate Yesu,Petro akajibu mashambulizi kwa kumkata sikio,lakini Yesu akamponya sikio lake na akamruhusu aendelee na ubaya wake.(yohana 18:10 na luka22:50-51.)hili pendo ni la tofauti halifanani na halielezeki,Na ndilo analotuagiza Bwana wetu Yesu Kristo kuwapenda adui zetu kwa kiasi hicho hata wangepanga mabaya juu yako,wewe wapende,wakutengenezee kifo wewe wapende tu.maisha yako ni mali ya Mungu hakuna anaweza kuchukua kama umesimama kwa uaminifu kwa Mungu.
Mwenye kuhukumu ni Mungu tu na haki yako ipo mikononi mwake usitumie nguvu kujitetea kama petro,mwachie yeye mwenye kuhukumu.
Maisha ya Yesu ni kioo yapasa tuyaige.yeye hakupigana na adui kwa jinsi ya mwili nasi tufuate mfano wake.Pia Paulo anazidi kusisitiza kuwa vita yetu ni ya ulimwengu wa Roho(efeso 6:12)

(b)kubariki wanaotuudhi(warumi 12:14 na mathayo 5:44)
Tumeagizwa kubariki si kulaani,vinywa vyetu viponye.Watu wengine wanatumia mamlaka vibaya wengine utamka maneno ya laana katika madhabahu,hilo ni kosa kubwa.Yesu walimdhihaki wakamnena mabaya mpaka msalabani jibu alilosema"Baba uwasamehe hawajui watendalo",kipimo cha kujua kinywa cha mkristo kimejaza nini ni wakati wa jaribu.Wengine wanatoa matusi,maneno ya laana,lawama kuonyesha kuwa vinywa vimejaa uchafu.Bwana atakase kinywa chako wakati wote.maneno yako yawe heri na baraka kwa wengine.

(c)kuwatendea mema wanaotuchukia.
Yesu akasema akunyang'anyae kanzu mpe na joho(mathayo 5;40).Mtendee mema adui yako,akiumwa mpeleke hospital,akiwa na njaa mpe chakula.

(d)kuwaombea wanaotuudhi na kututesa.
Kama Yesu alivyowaombea nasi tuige mfano wake.Tusiwatakie mabaya lengo letu kubwa au ombi langu maadui zangu waokoke na wamjue Mungu ninayemwabudu simpangii Bwana waokoke lini lakini najua ipo siku wataokoka.Na Mungu ndiye aliyeumba mbaya na mwema na malipo ya mbaya anayo yeye,namwachia mwenye kuhukumu.Tusishindwe na ubaya wala tusiwe na kisasi(zab.34:13-14.)

TABIA NNE ZA  MATENDO YA BINADAMU
(a)mtu akikutendea mabaya na ukalipa mabaya huo ni ubinadamu(wanadamu wengi wanalipa baya kwa baya)
.(b)mtu akikutendea mema na ukalipa mabaya huo ni ushetani au uibilisi.(atendaye hayo anakuwa amerithi tabia ya shetani)malipo ya shetani hata ungemfurahisha kwa kumtumikia kwa nguvu mwisho wake ni kukuangamiza tu hawezi hata siku moja akakulipa mema kusudi lake tangu mwanzo ni kuua,kuchinja na kuharibu.Anaweza akakuvutia lakini hana nia njema ni kama mtu anayefuga kuku wa nyama.atawahudumia vizuri kuku,anawapa chakula,madawa wakiugua pengine kuku anaweza kuwaza huyu mtu ananipenda kumbe sivyo matokeo ya mwisho ya hao kuku ni kuchinjwa tu.usifanye urafiki na shetani kuna siku atakumaliza tu hata akufurahishe kuna siku atakuchinja.ACHANA NAYE KWA JINA LA YESU. 
(c)mtu akikutendea mabaya wewe ukalipa mema huo ni ukiUngu( au hiyo ndiyo tabia ya KIMUNGU. Na ndivyo biblia inaagiza juu ya adui zetu.atendaye hayo anapata thawabu kubwa kwa Mungu.Japo wanadamu wanaweza kukuona mjinga lakini mbele za Mungu una maana kwa tendo hilo. 
(d)ukitenda mema kwa mema huo ni ukiUngu au tabia apendayo Mungu japo ni tabia ambayo wanadamu wengi utenda pia(haiwezi kufanana na ile ya kulipa mema kwa aliyekutendea mabaya.kipimo cha mtu aliyeokoka kipo hapo na ni wachache wanaoshinda.

Mchungaji:Lugano Mwakisole
EAGT Paradise Mbagala Zakhem


No comments:

Post a Comment

Andika maoni yako hapa

Note: Only a member of this blog may post a comment.