EAGT PARADISE ni kanisa la Kipentekoste lililo chini ya EAGT, Kanisa hili lipo Mbagala Zakhem,karibu na viwanja vya wazi Zakhem(Kwa watengeneza masofa), PARADISE linaongozwa na Mtumishi wa Mungu Mchungaji Lugano Mwakisole.
Sunday, August 31, 2014
Wednesday, August 27, 2014
KUWA RAFIKI WA KARIBU WA YESU-Mch.Lugano Mwakisole
MCHUNGAJI LUGANO MWAKISOLE |
KUWA RAFIKI WA KARIBU WA YESU
Kuna utofauti mkubwa kuwa
rafiki na mwanafunzi,
Kuwa rafiki wa Yesu ni zaidi
ya kuwa mwanafunzi wake,Ni kiwango ambacho si rahisi kwa mwamini kufikia kuwa
rafiki wa Karibu wa Yesu,Ni hatua ya juu sana
Ukiwa rafiki wa Yesu unapata
nafasi ya kuongaea na nae ana kwa ana,
Katika Somo hili tutajifunza
Jinsi Gani sisi kama wanafunzi wa Yesu tunaweza kuwa Rafiki zake wa
karibu.Fuata nami na Mungu atakubariki
HATUA ZA KUWA RAFIKI WA YESU.
1.UTII
hatua hii ni ya muhimu sana
ili ufikie kuwa rafiki.Yesu amesema ninyi mmekuwa rafiki zangu mkitenda
niwaamuruyo(Yohana 15:14),Yesu anathibitisha kuwa ili tuwe marafiki zake ni
lazima tutii maagizo yake..kipimo cha kumpenda Yesu ni kutii maagizo
yake.pia katika Yohana 14:21 inasema "Yeye aliye na amri zangu, na
kuzishika,yeye ndiye anipendaye;naye anipendaye atapendwa na Baba yangu,nami
nitampenda na kujidhihirisha kwake" mtu anayeshika amri au maagizo ya Yesu
ndiye ependwaye na Yesu au anakuwa rafiki wa Yesu.Yesu alimuuliza Petro mara
tatu kama kweli anampenda.(Yohana 21:15-17),Petro alipojitetea kwa sababu
nyingi na kutaka kuonyesha kuwa anampenda Yesu alimjibu kuwa achunge na kulisha
kundi.Kumbuka alimuuliza maswali haya baada ya kufufuka akisikitishwa na Petro
kuacha kutii wito aliomwachia kabla ya kufa na malezi yote aliyompa kwa
muda wote aliokaa naye.pia alipomwita aliwambia aache kuvua samaki naye
atamfanya kuwa mvuvi wa watu.Muda mfupi tu Yesu alipomwacha ameacha kutii agizo
ameenda kuvua samaki.kitendo cha kutokutii wito Yesu akahuzunika sana na
kumuuliza kweli anampenda? Tatizo ni kutokutii ndicho Yesu kilichomsononesha.Pia
lazima tujiulize mbona anaulizwa Petro si wanafunzi wengine?wakati kwenye kuvua
samaki walikuwa wengi,Jibu ni hili Yesu hakutegemea rafiki yake mpendwa au mwanafunzi
wa karibu zaidi ndio kaharibu.Ukiwa rafiki wa Yesu ni lazima uwe na utii wa hali
ya juu katika maagizo ndipo Yesu atakuwa na imani nawe.usifanye kitu
kitakachosababisha Yesu kuwa na mashaka na urafiki wenu kama Petro.Mimi na wewe
tujiulize je tumesimamia wito wetu na kutii kila agizo ili Yesu atupende
kama rafiki zake?
2.KUPENDA KUJIFUNZA
Hii ni hatua ya muhimu na
Yesu anaizingatia sana kwa marafiki zake.(Yohana 8:31) Yesu anasema “ninyi
mkishika neno langu mmekuwa wanafunzi wangu kwelikweli” kuwa mwanafunzi
kwelikweli kwa maana nyingine ni kuwa mwanafunzi anayepita wanafunzi wengine au
kuwa rafiki wa karibu.Tuna mfano wa dada aliyekuwa rafiki sana wa Yesu anaitwa
Mariam.alikaa miguuni pa Yesu akijifunza.(luka 10:38-42) Yesu alimpenda na
akasema amechagua fungu jema,na kihistoria anaonyesha ni miongoni mwa rafiki wa
karibu wa Yesu.Sehemu nyingi zinaonyesha kama kufa kwake,kufufuka kwake,na mpaka
anapaa alikuwa karibu naye sana.
3.HATUA YA UTOAJI
Hii ni sadaka ya tofauti na sadaka
ya kawaida.sadaka ambayo inamgusa Yesu kwa kiwango cha juu.Sadaka ambayo Yesu
akiangalia inamkumbusha sadaka yake kubwa aliyoitoa msalabani.ukitoa sadaka ya
namna hiyo ni lazima Yesu awe rafiki yako.sadaka hiyo inakufanya wewe
uchukuliwe uwe karibu na sadaka ya msalaba.Watu wengi waliotoa kwa kiwango cha
juu kama hicho waliugusa moyo wa Yesu na kuwa marafiki zake.
-Mfano wa kwanza ni baba wa
imani Ibrahim alikubali kumtoa mwanawe wa pekee Isaka kuwa sadaka ya
kuteketezwa.kitendo cha kutoa mtoto wa pekee ,mpendwa,kilimkumbusha Mungu
kumtoa mwanawe wa pekee Yesu kufa msalabani. Unaweza kusema mbona wakati huo
Yesu alikuwa bado hajafa.kumbuka mpango wa Yesu kufa ulipangwa na Mungu zamani
sana biblia inasema kabla ya kuwekwa misingi ya dunia(1petro1:19-20) kwahiyo
utoaji wa Ibrahim ulikuwa utabiri wa Yesu na ulimfanya Ibrahim kumkumbusha
Mungu sadaka yake.habari yote unaipata katika kitabu cha mwanzo 22.sura
yote.Pia tunaona katika msitari wa 11-12 malaika wa Bwana anamsifia Ibrahim kwa
moyo wake wa kumcha Bwana.Mungu aliuona moyo wa Ibrahim baada ya kutoa sadaka
ya tofauti.urafiki wa MUNGU na Ibrahim uliongezeka.
Mstari wa 13 Mungu
anatoa kondoo badala ya Isaka,hapa inafundisha kuwa yeyote atakayetoa kwa kiwango
cha juu na sadaka ya pekee,maalumu au inayogusa moyo wake Mungu lazima atoe
mbadala kwa lugha nyingine Mungu atakulipa kwa njia tofauti kama Ibrahim
alivyolipwa
(mst 15-18)
-Mfano mwingine ni Mariam Magdalena.pamoja
na kukaa miguuni pa Yesu na kujifunza lakini pia alimtegemeza Yesu kwa mali
zake.kuna sadaka moja ilimgusa Yesu,alipompaka Yesu kwa mafuta ya
thamani.katika desturi ya wayahud kulikuwa na kutawadha miguu na hii ilikuwa kwa
mtumwa kutawadha Bwana wake.Mariam hakutumia kitambaa,yeye akatumia
nywele za kichwa chake,pia wengine walitumia maji lakini yeye alitumia machozi
yake na mafuta ya thamani.(Yohana 12:3 na luka7:36-38)kitendo hiki kiligusa
moyo wa Yesu na kilimshangaza,mafuta thamani kubwa kumtawadha Yesu,ni sadaka kubwa
sana alitoa.Unyenyekevu wa Mariam(kudondosha machozi ishara ya maombi na
kumfuta kwa nywele zake kuonyesha kushuka),sadaka yake kubwa(kitendo cha
kutojari mali zake kwaajili ya Yesu)na kupenda kukaa miguuni pa Yesu na
kujifunza kilifanya Yesu awe rafiki yake zaidi ya wanafunzi wengine.
Bado kuna hatua nyingine tatu
ili kukamilisha kuwa rafiki wa Yesu,tutaendelea nazo wiki ijayo siku kama
hii.Ombi langu tafuta kuwa rafiki wa Yesu utapata faida nyingi ambazo
utazifahamu utakapoendelea na somo mpaka mwisho.
MUNGU AWABARIKI.
Mchungaji:Lugano Mwakisole
EAGT Paradise Mbagala Zakhem
Tuesday, August 26, 2014
Monday, August 25, 2014
IBADA YA JUMAPILI 24.8.2014 KATIKA PICHA
Mtumishi wa Mungu Majaliwa akimtukuza Mungu kwa wimbio wake "KWA MSAADA WA ROHO" |
Mama Mchungaji akimtumikia Mungu kwa njia ya Uimbaji |
Kwaya ya Kanisa ikihudumu |
Kwaya ya Kanisa ikihudumu |
Kwaya ya Kanisa ikihudumu |
Kwaya ya Kanisa ikihudumu |
Kwaya ya Kanisa ikihudumu |
Mzee wa Kanisa Shedrack |
Mtumishi wa Mungu,Mch.Lugano Mwakisole akileta kusudi la Mungu kwa Kusanyiko |
Wakati wa Maombezi |
Wednesday, August 20, 2014
Tuesday, August 19, 2014
AGANO JIPYA JUU YA ADUI ZETU-Mch.Lugano Mwakisole
MCHUNGAJI LUGANO MWAKISOLE
AGANO JIPYA JUU YA ADUI ZETU.
(Math.5:43-47)
Leo
ninapenda tushirikishane mtazamo wa agano jipya juu ya adui zetu.
Mtazamo wa
agano la kale na agano jipya ni tofauti.Agano la kale(torati)kwa sehemu
linasema jino kwa jino au linaruhusu kulipa baya kwa baya lakini ni
tofauti na agano jipya linaagiza kuwatendea mema adui zetu.Si kwamba biblia
inapingana,kila watu walipewa maagizo na namna ya kuishi kwa wakati wake.sisi
tupo kipindi cha agano jipya na maagizo ya Yesu aliyoyatoa ni tofauti na ya
kale.
Maagizo tuliyopewa ni magumu zaidi na hii inatokana na pia tuna uwezo
mkubwa wa kushinda sababu tuna neema zaidi kutokana na ukombozi wa Yesu pia
tuna Roho Mtakatifu aliyemwagwa kwa wote tofauti na zamani ilikuwa kwa watu
maalumu.Daudi aliweza kusamehe na kumpenda adui yake sababu alikuwa na Roho
mtakatifu lakini ilikuwa ngumu kwa wafuasi wake kuelewa sababu walihishi kwa
sheria na kufuata maongozi ya Daudi lakini wenyewe hawakujazwa Roho.Tofauti na
sasa kila mtu amejaa Roho hivyo anawezeshwa kushinda vikwazo na kusamehe pia
kuwapenda adui kutokana na nguvu ya Roho mtakatifu iliyo ndani yetu.(waefeso
3;20)Si vema katika vipengele vigumu kukwepa maagizo ya agano jipya na kukimbilia
la kale ili kujifariji.Wengi wetu wanalipa kisasi na kujitetea kupitia maandiko
na wengine wanalaani na kutoa maneno ya laana pengine hata madhabahuni na
kutafuta maandiko ya kuwafariji.Biblia yapasa kuielewa kwa upana na kujifunza
kwa umakini,si kila andiko utalitumia kwa wakati huu.mengine yaweza kusomwa
kama historia au unabii uliopita,mengine ni ya sasa na yanahitaji kutekelezwa
na mengine ni unabii ujao yapasa uyajue lakini usitumie kwa sasa kama
utekelezaji utasababisha ajali katika uliwengu wa roho.Lakini yote tumewekewa
ili tujifunze na tukiyaelewa yatatufaa.
Mtazamo wa sasa juu ya adui zetu ni;
(a)kupenda adui zetu(mathayo 5;44)
Upendo wetu tunarithishwa na Yesu.aliwapenda adui hata siku
moja mbaya wake amebeba panga ili amkate Yesu,Petro akajibu mashambulizi kwa
kumkata sikio,lakini Yesu akamponya sikio lake na akamruhusu aendelee na ubaya
wake.(yohana 18:10 na luka22:50-51.)hili pendo ni la tofauti halifanani na
halielezeki,Na ndilo analotuagiza Bwana wetu Yesu Kristo kuwapenda adui zetu kwa kiasi hicho hata
wangepanga mabaya juu yako,wewe wapende,wakutengenezee kifo wewe wapende
tu.maisha yako ni mali ya Mungu hakuna anaweza kuchukua kama umesimama kwa
uaminifu kwa Mungu.
Mwenye kuhukumu ni Mungu tu na haki yako ipo mikononi mwake
usitumie nguvu kujitetea kama petro,mwachie yeye mwenye kuhukumu.
Maisha ya Yesu
ni kioo yapasa tuyaige.yeye hakupigana na adui kwa jinsi ya mwili nasi tufuate
mfano wake.Pia Paulo anazidi kusisitiza kuwa vita yetu ni ya ulimwengu wa
Roho(efeso 6:12)
(b)kubariki wanaotuudhi(warumi 12:14 na mathayo 5:44)
Tumeagizwa kubariki si kulaani,vinywa vyetu viponye.Watu wengine wanatumia mamlaka vibaya wengine utamka maneno ya laana katika madhabahu,hilo
ni kosa kubwa.Yesu walimdhihaki wakamnena mabaya mpaka msalabani jibu
alilosema"Baba uwasamehe hawajui watendalo",kipimo cha kujua kinywa cha
mkristo kimejaza nini ni wakati wa jaribu.Wengine wanatoa matusi,maneno ya
laana,lawama kuonyesha kuwa vinywa vimejaa uchafu.Bwana atakase kinywa chako
wakati wote.maneno yako yawe heri na baraka kwa wengine.
(c)kuwatendea mema wanaotuchukia.
Yesu akasema akunyang'anyae kanzu mpe na joho(mathayo
5;40).Mtendee mema adui yako,akiumwa mpeleke hospital,akiwa na njaa mpe chakula.
(d)kuwaombea wanaotuudhi na kututesa.
Kama Yesu alivyowaombea nasi tuige mfano wake.Tusiwatakie
mabaya lengo letu kubwa au ombi langu maadui zangu waokoke na wamjue Mungu
ninayemwabudu simpangii Bwana waokoke lini lakini najua ipo siku wataokoka.Na
Mungu ndiye aliyeumba mbaya na mwema na malipo ya
mbaya anayo yeye,namwachia mwenye kuhukumu.Tusishindwe na ubaya wala tusiwe na
kisasi(zab.34:13-14.)
TABIA NNE ZA MATENDO YA BINADAMU
(a)mtu akikutendea mabaya na ukalipa mabaya huo ni
ubinadamu(wanadamu wengi wanalipa baya kwa baya)
.(b)mtu akikutendea mema na ukalipa mabaya huo ni ushetani
au uibilisi.(atendaye hayo anakuwa amerithi tabia ya shetani)malipo ya shetani
hata ungemfurahisha kwa kumtumikia kwa nguvu mwisho wake ni kukuangamiza
tu hawezi hata siku moja akakulipa mema kusudi lake tangu mwanzo ni
kuua,kuchinja na kuharibu.Anaweza akakuvutia lakini hana nia njema ni kama mtu
anayefuga kuku wa nyama.atawahudumia vizuri kuku,anawapa chakula,madawa
wakiugua pengine kuku anaweza kuwaza huyu mtu ananipenda kumbe sivyo matokeo ya
mwisho ya hao kuku ni kuchinjwa tu.usifanye urafiki na shetani kuna siku
atakumaliza tu hata akufurahishe kuna siku atakuchinja.ACHANA NAYE KWA JINA LA
YESU.
(c)mtu akikutendea mabaya wewe ukalipa mema huo ni ukiUngu(
au hiyo ndiyo tabia ya KIMUNGU. Na ndivyo biblia inaagiza juu ya adui
zetu.atendaye hayo anapata thawabu kubwa kwa Mungu.Japo wanadamu wanaweza
kukuona mjinga lakini mbele za Mungu una maana kwa tendo hilo.
(d)ukitenda mema kwa mema huo ni ukiUngu au tabia apendayo
Mungu japo ni tabia ambayo wanadamu wengi utenda pia(haiwezi kufanana na ile ya
kulipa mema kwa aliyekutendea mabaya.kipimo cha mtu aliyeokoka kipo hapo na ni
wachache wanaoshinda.
Mchungaji:Lugano Mwakisole
EAGT Paradise Mbagala Zakhem
Monday, August 11, 2014
BARAKA ZETU ZIPO KATIKA NENO.
MATHAYO 4 :4 "mtu hataishi kwa mkate tu
bali kwakila neno litokalo katika kinywa
cha Mungu"
Wapendwa wasomaji napenda tushirikishane jambo kuu sana lina
lohusu baraka.kila mtu anapenda baraka lakini ni muhimu kufahamu msingi wa
baraka zetu tuliookoka unapatikana wapi,na wenzetu au mababa zetu wa Imani katika biblia
walipata baraka kupitia nini?soma zaidi upate kuelewa.
KUNA TOFAUTI YA KUFANIKIWA NA KUBARIKIWA.
Mafanikio ni matokeo ya mwilini bali baraka zinaanza rohoni
nakuonekana mwilini.Mtu aliyefanikiwa anaweza akawa na pesa,magari,majumba ya
kifahari(matokeo ya nje) lakini akawa hana amani,furaha ya ki Mungu na upendo wa
ki Mungu.pia ni mtu anayeishi kwa masharti mazito,na hofu tele juu ya utajiri
wake,hii tena si baraka bali ni mafanikio tu,baraka ni matokeo ya rohoni kwanza
inayobeba furaha,amani na upendo wa ki Mungu.Baraka inaanza rohoni kwa vitu
hivyo nilivyovitaja(upendo,furaha na amani ya kiMungu) ndipo inadhihirika
mwilini kama matokeo ya utajiri wa fedha,nyumba,magari nk.Mtu akipata vitu vya
mwilini akakosa amani na vitu hivyo au furaha ya Mungu anakuwa ni mtu wa
huzuni,anakosa upendo na ndugu zake au marafiki,mara nyingine anakuwa na ukali
usio na sababu, msongo wa mawazo japo ana kila kitu.Anapungukiwa na baraka au
vitu vya ndani (rohoni)vitakavyomfurahisha kwanza bali vinavyoonekana na
matokeo yake yanakuwa ni mabaya.Anaweza kuacha vyote na ukashangaa analala kwa
mganga wa kienyeji au mpunga pepo,katika mazingira machafu yasiyoendana na
yeye.tatizo alidhani baraka zinaanzia mwilini kumbe baraka zinaanza rohoni na
kumalizikia mwilini.maandiko yanasema"utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na
haki zake na mengine tutazidishiwa"Haki zinazosemwa hapo ndio hizo furaha
amani pendo za kiMungu na mengine tunayozidishiwa ni utajiri tunaouona kama
fedha, magari,majumba n.k Na baraka zetu zinajengwa na neno la Mungu na huu
ndiyo msingi wetu.
Maisha yetu,kuishi kwetu,kula yetu,vaa
yetu na baraka zetu zimebebwa katika neno.
Na hii ndio maana ya kusema tunaishi kupitia
neno analosema Mungu.(math 4:4).Pia andiko la EBRANIA
10 : 38 linasema "mwenye haki wa mungu ataishi kwa imani"
inapoongelewa imani inamaanisha kusikia neno la kristo ,(WARUMI 10
:17) Hapo tunapata picha zaidi kuwa maisha yetu yote
na mafanikio yamebebwa na neno la Mungu:
Neno humjenga mtu katika imani na imani
inasababisha baraka zote za kimwili na kiroho.watu wengi wanapenda
kubarikwa lakini hawataki kuishi kwa neno,kulisoma neno,au kusikia
kupitia watumishi wa Mungu.Hawaendi kanisani kukutana na mtoa baraka kwa
kisingizio wana kazi nyingi. Ni vigumu watu hawa kupata baraka za
kiMungu.Baraka huja kupitia neno la Mungu, unapolisikia na kulitendea
kazi , na Baraka inaanzia rohoni ndipo hudhihirika
mwilini .Yohana aliandika waraka wake " 3YOHANA 1 :2 mpenzi naomba
ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na Afya njema kama vile roho yako
ifanikiwavyo" akiwa anamanisha baraka zote zinaanza rohoni
ndipo inadhihirika mwilini
MIFANO YA WATU WALIOBARIKIWA KUPITIA NENO LA MUNGU.
1. Ibrahimu baba wa imani(MWANZO 12:1-3)
Ibrahimu aliambiwa neno na Mungu atoke aende katika
nchi ambayo aliandaliwa baraka tele.
Baraka zilianza pale tu Ibrahimu alipotii neno au agizo na
akatekeleza.mstari wa 4 ibrahim alitekeleza na alipotoka baraka zilimfuata kama
neno liliivyomwambia.japo alipitia mitihani mingi lakini ushindi wa mwisho
ulikuwa mkuu sana na matokeo yake ni makubwa,Tunaona matokeo ya taifa la israel
ni kutokana na kutii kwa ibrahim.ishi kwa neno na kutii kama Ibrahim utaziona
baraka kwako na familia yako na hata kizazi chako chote.
2 NABII ELIYA: WAFALME 17 :1-16
Hapo tunaona maisha alioishi Eliya baada ya kutokea njaa iliyosababishwa na maombi yake mwenyewe. Baada ya kuzuia mvua kulikuwa na ukame na njaa kubwa katika mji wa israeli wakati huo mgumu watu wengi walisumbuka sana kutafuta chakula lakini Eliya kwake maisha hayakuwa magumu sababu yeye aliishi kwa neno la Mungu.
Hapo tunaona maisha alioishi Eliya baada ya kutokea njaa iliyosababishwa na maombi yake mwenyewe. Baada ya kuzuia mvua kulikuwa na ukame na njaa kubwa katika mji wa israeli wakati huo mgumu watu wengi walisumbuka sana kutafuta chakula lakini Eliya kwake maisha hayakuwa magumu sababu yeye aliishi kwa neno la Mungu.
Ukisoma mstari 2-7 Neno lilimjia Eliya
aende katika kijito cha kerithi. Alipotii kwenda huko Mungu
alikuwa amemwandalia kunguru wamlishe katika kijito hicho na kunywa
maji hayo. wakati huo mgumu , Eliya haukumsumbua kwasababu
yeye alitii neno la Bwana na aliweza kuishi.Hali ngumu za maisha au
kukosa pesa si sababu ya kukata tamaa kwani tukiamini neno lake,Mungu atafungua
njia juu yetu.kumbuka neno linasema "dunia na vyote viijazavyo ni mali ya
Bwana,ZABURI 24:1.Pia anatupa ahadi kuwa tukimwomba yeye atatupa kwa kuwa na
sisi ni watoto wake.(MATH 7:7-11)
Mstari 8:16 katika 1wafalme 17 tumeona kijito
kilikauka kutokana na hali ya ukame, lakini hilo
halikumtisha Eliya bali alisikiliza maelekezo ya neno.
Ndipo neno likamwongoza kwenda kwa mwanamke mjane wa serepta na akafanya
muujiza kupitia mafuta kidogo katika chupa na unga kidogo. Na muujiza
mkubwa ukafanyika wakaishi.
Eliya hakutishwa na mabadiliko ya hali ya hewa
bali aliamini neno kuwa litamfanya aishi . Je ni kitu gani kinakufanya
uwe na hofu ya maisha, je kukosa kazi, mabadiliko ya uchumi, au kukataliwa na
ndugu au jamaa.? Vyote hivyo haviwezi kuzuia baraka zetu sababu sisi hatuishi
kwa bahati(hatubahatishi maisha) bali maisha yetu yanaongozwa na
neno (MATHAYO 4:4).Watu wasiookoka wanaishi kwa bahati na ndio maana wanaishi
kwa wasiwasi na wengine husema "bahati hairudi mara mbili"sababu
wanabahatisha wanakuwa na hofu wakifilisika utakuwa ndio mwisho wao.Sisi
tuliookoka tunaishi kwa neno au maongozi ya neno na baraka zetu ni nyingi hata
zikizuiliwa na shetani au watu wenye hila sehemu fulani,iwe kufukuzwa
kazi,kudhurumiwa,kutendewa mabaya na watu tuliowaamini lakini
wakageuka,bado Mungu atafungua kwa njia nyingine. Sisi ni wabarikiwa na ni
kipawa tulichopewa kama biblia isemavyo"kipawa ni kito cha thamani na kila
kigeukapo hufanikiwa,)Maana ya kila kigeukapo inamaanisha kila uendapo na kila
ufanyacho utafanikiwa.Shetani japo alijaribu kugusa maisha ya Ayubu kwa
magonjwa,kuuwa watoto wake na mifugo na mali zake kufilisiiwa,bado alimtegemea
Mungu na matokeo ya mwisho yalikuwa mazuri kuliko mwanzo na alipata utajiri
mwingi kuliko mwanzo.Hata kama shetani alichezea uchumi wako na ukakata
tamaa,nakutia moyo kuwa baraka yako bado ipo si za kubahatisha,Yesu atakubariki
kwani anazo baraka nyingi.Pia baraka zetu zinatufuata popote tunapoenda kama
neno lisemavyo " hakika wema na fadhiri zitatufuata siku zote
za maisha yetu, ZABUR 23:6"
Pia baraka zetu anayetoa ni Mungu na ndie anatupa nguvu za
kupata utajiri( KUMB 8:17:18) Wala si uwezo wetu hivyo tumtegemee
yeye ambae ndiye neno (YOHAN 1:1) Ili atupe mahitaji yetu,
Vitu vyote vipo chini yake na anatoa kwakila mtu anaye
mcha na kumtii( 1MAMB NYKT 29:12).
Ushauri wangu kwako mpe Yesu maisha yako utapata baraka za Bwana ambazo zinajumuishwa na upendo,furaha,na amani kisha utajiri wa fedha,mifugo,mashamba,majumba,magari n.k Bwana atatuzidishia na baraka ya Mungu inaenda hatua kwa hatua,yapasa uwe mvumilivu kama baba yetu Ibrahim aliyepita wakati mgumu lakini mwisho wake ulikuwa mzuri.Usitake utajiri kwa haraka dunia itakupoteza.wengi tunawaona walitaka utajiri kwa haraka lakini wamekufa mapema tena kwa vifo vya kuhuzunisha na pesa na utajiri wao hawakuufaidi bali wamefaidika wengine.Baraka ya Mungu hutajirisha na haichangamani na majuto.Mungu awabariki.
Kwa Msaada Zaidi
Waweza kuwasiliana nami
0688387834
luggymakky@gmail.com
Ushauri wangu kwako mpe Yesu maisha yako utapata baraka za Bwana ambazo zinajumuishwa na upendo,furaha,na amani kisha utajiri wa fedha,mifugo,mashamba,majumba,magari n.k Bwana atatuzidishia na baraka ya Mungu inaenda hatua kwa hatua,yapasa uwe mvumilivu kama baba yetu Ibrahim aliyepita wakati mgumu lakini mwisho wake ulikuwa mzuri.Usitake utajiri kwa haraka dunia itakupoteza.wengi tunawaona walitaka utajiri kwa haraka lakini wamekufa mapema tena kwa vifo vya kuhuzunisha na pesa na utajiri wao hawakuufaidi bali wamefaidika wengine.Baraka ya Mungu hutajirisha na haichangamani na majuto.Mungu awabariki.
Kwa Msaada Zaidi
Waweza kuwasiliana nami
0688387834
luggymakky@gmail.com